Haya ni kwa mujibu wa makala iliyochapishwa na tovuti ya Al-Muslimun Hawl al-Alam kuhusu tafsiri na tarjuma za Kibosnia za Qur'ani Tukkufu, ambazo sehemu zake ni kama zifuatazo:
Kibosnia ni miongoni mwa lugha za Kislavoni cha Kusini ambazo zimeboreshwa zaidi kuliko Kikroeshia na Kiserbia kwa sababu ya mwingiliano wake wa kitamaduni na Kituruki cha Wauthmaniya
Kumekuwa na tarjuma nyingi za Qur'ani katika Kibosnia, ambazo zote kwa pamoja ni katika juhudi za kuwasilisha dhana na maana kwa usahihi.
Uchunguzi kuhusu tarjuma za awali unaonyesha kwamba lengo kuu lilikuwa kwenye maana, lakini kadiri muda ulivyosonga, watafsiri walitilia maanani zaidi kugundua maadili ya kifasihi na kimuundo ya matini pia.
Tarjuma ya kwanza ya Kibosnia ya Qur'ani Tukufu ilifanywa na asiye Mwislamu, kasisi wa Kanisa la Orthodox Mihajlo Mićo Ljubibratić.
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika kurasa 479 mnamo 1895, baada ya kifo cha Ljubibratić, na kisha kuchapishwa tena mnamo 1990.
Kwa tarjuma hii, alitaka kuwaleta Waislamu na Waserbia Wakristo karibu zaidi na kukuza mazungumzo na maelewano kati yao.
Alitegemea tarjuma kadhaa za Qur'an ya Kifaransa na Kirusi katika tarjumai yake, ambayo ina makosa mengi.
Tarjuma iliyofuata ilikuwa ya wanazuoni wawili wa Kiislamu walioitwa Jamaleddin Jashvic (1870-1932) na Al-Hafiz Mohamed Banja (aliyefariki 1962). Ilikaribishwa na watu na wasomi wa Bosnia ilipochapishwa mnamo 1937.
Wawili hao walitegemea tarjuma na tafsiri za Kiajemi, Kituruki na Kitatari katika kazi yao, ambayo nayo pia ilikuwa na makosa. Tarjuma yao ilichapishwa tena mara kadhaa.
Tarjuma nyingine pia iliyochapishwa mwaka 1937 ilikuwa ya Mufti wa Herzegovina Haj Ali Ridha Qarabac (aliyefariki 1944). Ilikuwa ni tarjuma dhaifu iliyo na makosa mengi.
Wakati Bosnia ilipokuwa sehemu ya Yugoslavia, watawala walikataa kutambua lugha ya Kibosnia na hawakuruhusu itumiwe kati ya 1945 na 1990.
Katika kipindi hiki, tafsiri moja tu ya Qur'ani katika lugha hii ilikuwa ya Profesa Besim Korkut (1904-1975), ambaye alikuwa mhitimu wa Chuo Kikuu cha Al-Azhar cha Misri.
Katika tarjuma yake, alitegemea sana Tafsiri ya Qur'ani ya Al-Kashshaaf ya Al-Zamakhshari.
Tarjuma hiyo ilichapishwa mwaka wa 1977, baada ya kifo cha Korkut. Tarjuma hiyo imesifiwa kwa kuwa karibu na maana ya aya za Qur'ani Tukufu
Kulikuwa na tarjuma zaidi za Qur'ani Tukufu zilizochapishwa nchini Bosnia baada ya nchi hiyo kupata uhuru kutoka kwa Yugoslavia mnamo 1990.
Moja ilikuwa ya Mustafa Mlivo (aliyezaliwa 1955), ambayo ilichapishwa mwaka 1994 na kuchapishwa tena mwaka mmoja baadaye katika kurasa 719.
Tarjuma nyingine ya Enes Karić (aliyezaliwa 1995) ilichapishwa mwaka wa 1995 na inachukuliwa kuwa miongoni mwa tafsiri nzuri za Kitabu Kitakatifu katika Kibosnia.
Tarjuma bora Zaidi ya Qur'ani Tukufu kwa lugha ya Kibosnia imetajwa kuwa ni ile ya Esad Duraković (aliyezaliwa 1948), ambaye alikuwa mkuu wa Idara ya Masuala ya Mashariki (Orientalism) ya Chuo Kikuu cha Sarajevo na mwanachama wa Akademia ya Kiarabu huko Damascus.
Tarjuma hiyo inayojulikana kama "Kuran s prijevodom", inachukuliwa na wataalamu kama tarjuma bora zaidi ya Qur'ani katika Kibosnia.
Duraković ni msomi wa ngazi za juu wa Bosnia wa Masomo ya Kiarabu na Kiislamu. Baada ya kuhitimu kutoka Chuo Kikuu cha Belgrade katika Yugoslavia ya zamani (sasa Serbia) mwaka wa 1972, Duraković alianza kazi yake ya kitaaluma huko Belgrade na Priština (Kosovo ya sasa), na aliandikaa tasnifu ya uzamivu kuhusu fasihi ya Kiarabu. Tangu 1991 Duraković amehusishwa na taasisi mbalimbali za kitaaluma huko Sarajevo.
Tarjuma yake ilikamilishwa mwaka wa 2002, na kuchapishwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2004, na imetajwa kuwa tarjuma za kisasa zaidi ya Qur'ani katika Kibosnia. Kinyume na tarjuma za awali, Duraković anasema amewasilisha maana halisi ya aya za Qur'ani.
Kwa mfano, anaona kuwa ni muhimu kufuata msuko wa balagha (al-iltifāt) wa matini asilia ya chanzo cha Kiarabu wakati wa kutafsiri. Katika utafiti mmoja, ambapo anaelezea mbinu yake ya katika tarjuma ya Qur'ani, Duraković anaandika kwamba '[Mfano wowote wa] Iltifat katika Qur'an, pamoja na kuwa na utendaji bora wa kimtindo, umejaa maana: Iltifat inabeba kiini cha ujumbe wa Qur'ani . Katika utangulizi wa tarjuma yake Duraković anafichua imani yake juu ya hitajio la tarjuma ya Qur'ani ambayo itatanguliza ufasaha wa maandishi asilia badala ya kujihusisha tu na masuala ya kitheolojia ‘kama walivyofanya watarjumi wengine hapo awali’.
Zana za kisanii anazotumia Duraković ili kufanikisha mbinu hii inaonekana kuwa ya kibunifu katika suala la tarjuma za Qur'ani za Kibosnia. Mtindo wa tarjuma hiyo unaifanya iweze kuwavutia wengi nchini Bosnia na maeneo jirani ya eneo la Balkan.
3490458